UHAKIKI WA RIWAYA YA VUTA N`KUVUTE BY SHAFI ADAM SHAFI (Teacher Hassan Lemunje)
KITABU- VUTA N’KUVUTE
MWANDISHI – SHAFI ADAM SHAFI
WACHAPISHAJI – MKUKI NA NYOTA PUBLISHERS
MWAKA – 1999
Utangulizi
Riwaya hii inazungumzia matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu kwa sasa. Matatizo hayo ni kama vile matabaka,Unyonyaji, umaskini, ndoa za kulazimishwa, wivu katika ndoa, na Mengineyo mengi..
Maudhui
Dhamira kuu: Ukombozi
Katika kujadili Suala la ukomboz mwandishi anaonesha Katika Nyanja kuu NNE ambazo ni:
1.UKOMBOZI WA KIFIKRA
Mfano Yasmini Kutoroka Utawani Inaashilia kuwa alikua amejikomboa kifikra na aliona kuwa anaonewa
2.UKOMBOZI WA KIUTAMADUNI.
Unajidhihirisha pale ambapo Yasmini Anapinga baadhi ya mila ikiwemo ile ya kuwekwa utawani na kulazimishwa kuolewa na mtu asiyemtaka hivyo Kupinga kwake ni ishara tosha ya UKOMBOZI WA kiutamaduni.
3.UKOMBOZI WA KISIASA
Unajidhihirisha kupitia Harakati za Denge na Kundi lake kutaka Kujikomboa na Kujitawala wenyewe.
4.UKOMBOZI WA KIUCHUMI.
Huu pia unadhihirishwa na Harakat za Kundi la Denge kujikwamua kutoka kwenye minyororo ya Ukoloni ili kuwa Huru na kumiliki Njia Zote za Udhalishaji Mali
#Dhamira Nyinginezo Tutakazo Jadili Katika Makala Hii ni Pamoja na#
>Usaliti
>Suala la Mapenzi
>Wivu
>Matabaka
>Umasikini
>Unyonyaji
>Huruma
>Nafasi ya mwanamke katika Jamii.
Migogoro
a)Yasmin v/s wazazi wake
b)Yasmin v/s Raza
c)Yasmin v/s Denge
d)Denge v/s serikali
e)Yasmin v/s Mwajuma
f)Yasmin v/s Koplo Matata
Msimamo
Mwandishi anaonesha msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha wazi kuwa jamii yetu ina baadhi ya mila na desturi zilizopitwa na wakati, hivyo jamii lazima izifutilie mbali.
Falsafa
Mtunzi anaelekea kuamini kuwa mapenzi ya kweli yatapatikana katika jamii ikiwa kutakuwa na uhuru wa kuchagua yule unayemtaka, badala ya kulazimishwa na wazazi.
Fani
Muundo
Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja. Anaanza masimulizi yake kwa kuelezea ndoa ya Raza na Yasmin, Yasmin kumwacha Raza, Yasmin kwa Mwajuma, Yasmin kuolewa na Shihab na mwisho ndoa ya Yasmin na Bukheti.
Mtindo
Mwandishi ametumia mtindo wa monolojia (masimulizi) kwa kiasi kikubwa ingawa pia kumejitokeza dayalojia. Katika kuukamilisha mtindo wake msanii pia ametumia barua (uk. 168), nyimbo (uk. 85-86). Pia nafsi zote tatu zimetumika.
Matumizi ya lugha
Mwandishi ametumia lugha rahisi inayoeleweka hata kwa msomaji wa kawaida, pamoja na misema, methali,tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.
Misemo/Nahau
a)Kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa (uk. 205)
b)Hujui kama mkono wa serikali ni mrefu (uk.71)
c)Wacha kutia chumvi (uk. 54)
d)Hana mbele wala nyuma (43)
e)Alipiga moyo konde (uk. 42)
f)Kuna dansa la kukata na shoka (uk.35)
g)Maji yamezidi unga (uk. 15)
Methali
a)Asiyekubali kushindwa si mshindani (uk. 271)
b)Mwangaza mbili moja humponyoka (uk. 230)
c)Mzoea punda hapandi farasi (uk. 207)
d)Heri nusu shari kuliko shari kamili (uk.42)
Tamathali za semi
Tashibiha
Bwana Raza amekaa juu ya kiti amevimba kama kiboko (uk. 9)
Kijana yule aliyekuwa na macho makali kama kurunzi (uk. 13)
Ametoa macho kama chui (uk. 31)
Yeye na ndani na ndani nay eye kama mwari (uk. 33)
Mweupe kama mgonjwa wa safura (uk. 82)
Tashihisi
Chumbani mle watu wakaanza, hawaonani na mbu wakaanza kujiandaa kwa karamu yao (uk. 194)
Nuru ya jua iliingia kwa hamaki chumbani mle na ilikashifu uchafu wote wa chumba kile (uk. 49)
Tabaini
Mabinti waliolelewa wakaleleka, waliofunzwa wakafunzika, waliotunzwa wakajitunza (uk. 85)
Hatua si hatua, mseto si mseto, ugali si ugali (193)
Sina shoga, sina jirani, sina jamaa, mimi na ndani na ndani na mimi, sirudi sirudi (uk. 211)
Mbinu nyingine za kisanaa
Takriri
Yeye hakuona isipokuwa Yasmin, Yasmin, Yasmin gani naye? (uk. 84)
Haweshi, ingia toka na kila wakija Denge, Denge na umewakosea nini hasa? (uk. 86)
Haya tunywe, tunywe kwa afya ya mgeni wetu (uk. 26)
Mjalizo
Raha ya kuwa karibu naye wakaongea, wakacheka, wakafurahi (uk. 14)
Kula mkate wa ufuta, mkate wa maji, mkate wa mayai (uk. 80)
Mdokezo
Naona siku hizi…….(uk. 15)
Unani…..(uk. 16)
Mbona unaogopa dada, unafikiri si……(uk. 25)
Halafu kanigaia shilingi ishirini na ……..(uk. 67)
Tanakali sauti (Onomatopea)
Oooooh, Yasmin alijilaza kitandani akapumua kwa machofu ya safari aliyokwenda (uk. 44)
Ngo, ngo, ngo, aligonga mlango (uk. 8)
Matumizi ya Kiingereza
Passing showa (uk. 17)
Brother, you fool (uk. 31)
Come on (uk. 32)
Mandhari
Riwaya hii imetumia mandhari halisi ya visiwa vya Unguja, maeneo ya Tanga na Mombasa –Kenya. Lakini matukio mengi yamefanyika Unguja. Vilevile kuna mandhari ya dukani, gerezani, baharini, nyumbani, mtaani, baa, klabuni, n.k
Jina la kitabu
Jina la kitabu linasadifu vizuri yaliyomo ndani ya kitabu hiki. Msanii anaonesha mivutano mbalimbali katika kitabu hiki.
Kwanza kuna mvutano kati ya Yasmin na wazazi wake. Huu unatokana na Yasmin kumwacha mume wake Raza ambaye wazazi wake walimlazimisha aolewe naye.
Pili, kuna mvutano kati ya Yasmin na Raza. Yasmin hakumpenda kabisa Raza, kwani kiumri Raza alikuwa ni sawa na baba yake wa kumzaa. Hivyo katika maisha yake ya ndoa na Raza wakawa na mivutano ya kila siku.
Tatu, kuna mvutano kati ya wakoloni na vijibwa vyao na wananchi wa kawaida wakiwakilishwa na Denge, Chande, Sukutua, Mambo na wengine. Hawa wanataka uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe, wanataka uhuru wa kumiliki njia kuu za uchumi badala ya wakoloni.
Nne, kuna mvutano kati ya Yasmin na Shihab. Huu unatokana na wivu wa kimapenzi. Shihab alikuwa na wivu sana kwa mke wake, matokeo yake akamnyima uhuru kwa kumweka utawani hatimaye Yasmin akamkimbia.
Mwisho, kuna mivutano ya kinafsia ambayo iliwahusu wahusika wenyewe. Hawa walikuwa na migongano ya kimawazo katika vichwa vyao. Mfano ni Yasmin, Bukheti, Denge, n.k
Kufaulu kwa mwandishi
– Mwandishi amefaulu sana kwa kuonesha mvutano wa vijana na wazee.
– Kifani amefaulu sana hasa katika uteuzi mzuri wa lugha na ujenzi wa wahusika. Lugha ni rahisi na inayoeleweka kwa kila mtu.
Kutofaulu kwa mwandishi
– Suluhisho la mgogoro kati ya wakoloni na wananchi halijaoneshwa, kwani tunaona tu wapigania uhuru wanawekwa ndani na wengine wanatoroka kwenda nje ya nchi. Je, hawa watu watatumia mbinu gani katika kujikomboa? Msanii hajaonesha.
– Matumizi ya lugha ya Kiingereza ni udhaifu mwingine wa msanii, kwani mtu asiyefahamu lugha hiyo hataweza kuelewa ujumbe uliomo kwa urahisi.
– Msanii hajaonesha mipaka ya uhuru unaotakiwa kwa watoto wetu. Kwa mfano, Yasmin ametumia uhuru wake wa kumchagua Shihab lakini naye ndoa yao haikudumu. Au uhuru wa Yasmin wa kuolewa na kuachika ndio uhuru unaotakiwa? Msanii hajaonesha vizuri.
Makala hii imeandikwa na:
Mwalim Mohamed Kahana
Contacts: 0715065259